Mumbai, Mei 30, 2020 - Ubalozi wa Tanzania nchini India, kwa kushirikiana na Shirika la Ndege la Tanzania [ATCL] pamoja na Diaspora wa Tanzania nchini India kwa mara nyingine wamefanikisha safari ya pili ya kuwarejesha nchini Watanzania waliokuwa wamekwama katika miji mbalimbali nchini India kutokana na zuio la kuingia na kutoka kwa ndege za Kimataifa lililowekwa na Serikali ya India kama hatua mojawapo ya kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.
Ndege maalum ya aina ya Boeng 787-8 ya Dreamliner ya Shirika la Ndege la Tanzania ilitumwa tena na Serikali Jijini Mumbai kuja kuwachukua Watanzania hao waliokwama nchini India tangu tarehe 22 Machi 2020 lilipowekwa zuio hilo na Serikali ya India. Ndege hiyo imeondoka leo tarehe 30 Mei 2020 saa 1 asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Chhatrapati Shivaji International Airport, Mumbai ikiwa imebeba jumla ya raia wa Tanzania 192, miongoni mwao ni waliokuwa wamekuja India kwa ajili ya matibabu; wahitimu kutoka vyuo mbali mbali na wanafunzi ambao wanalazimika kurudi nyumbani kwa kuwa vyuo vimefungwa hadi mwezi Agosti/Septemba 2020.
Tofauti na awamu ya kwanza safari hii pia ilihusisha kuwarejesha nchini India raia wa India wapatao 202 ambao walikuwa wamekwama nchini Tanzania. Hatua hii ya Serikali ya Tanzania itasaidia sana katika kuimarisha mahusiano mazuri yaliyopo kati ya India na Tanzania.
Mpaka sasa jumla ya Watanzania 438 wamerejeshwa Tanzania kutoka India kwa utaratibu huu maalum. Hata hivyo, takwimu zilizopo Ubalozini zinaonesha kuwa bado wapo Watanzania waliosalia nchini India kwa sababu mbalimbali na ambao wangehitaji huduma ya aina hii.
Aidha, zipo taarifa za Ubalozi wa India nchini Tanzania zinazoonesha kuwa wapo raia wa India ambao bado wamesalia nchini Tanzania na ambao wanahitaji kurejeshwa India.
Ndege iliyoondoka leo inatarajiwa kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere [JNIA] mnamo saa 7 mchana leo Jumamosi tarehe 30 Mei 2020.