New Delhi, 31 Oktaba 2019

Tanzania imeshiriki pamoja na nchi nyingine zipatazo 80 katika Mkutano Mkuu wa 2 wa Taasisi ya Kimataifa ya Nishati ya Jua (ISA) uliofanyika mjini New Delhi tarehe  30-31 Oktoba 2019.

Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda, ambaye alimwakilisha Waziri wa Nishati. Wajumbe wengine wa Tanzania; Bibi Natihaika Msuya-Afisa Mambo ya Nje katika ubalozi wa Tanzania New Delhi, Bw. Ngereja Mgejwa-Afisa Nishati Mwandamizi ambaye pia ni Katibu wa Naibu Waziri wa Nishati na Bw. Emilian Nyanda-Afisa Nishati Mwandamizi katika Wizara ya Nishati.

Katika hotuba yake, Balozi Luvanda, pamoja na mambo mengine aliwajulisha wajumbe wa Mkutano kuwa tarehe 29 Oktoba 2019, Baraza la Mawaziri limepitisha Azimio la kuridhia kujiunga na Taasisi ya ISA ili kuweza kuwa mwanachama kamili na hivyo kunufaika zaidi na huduma mbalimbali za taasisi hiyo katika masuala ya kujengea uwezo wataalam wa nishati ya jua na kubadilishana teknolojia na vifaa.

Aidha, alieleza kuwa hatua inayofuata ni kwa kwa mkataba huo kuwasilishwa bungeni kwa ajili ya kuridhiwa na kukamilisha mchakato wa uanachama wa Tanzania katika taasisi hii muhimu.

Tanzania iliweka saini mkataba wa uanzishwaji wa ISA mwezi Novemba, 2016 katika mkutano uliofanyika huko Marrakech, Morocco.

ISA ni taasisi iliyoanzishwa kwa msukumo wa Serikali ya India na Ufaransa na Makao Makuu yako Jijini New Delhi. Mpaka sasa nchi 89 ndizo zimesaini mkataba wa kuanzishwa kwa taasisi hii na nchi 59 zimesharidhia mkataba huu.