Mumbai, Februari 05, 2020- Ubalozi wa Tanzania, New Delhi, Taasisi za Serikali na kampuni binafsi mbalimbali za utalii nchini zinashiriki Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Mwaka 2020 nchini India yajulikanayo kama OTM 2020 [Outbound Travel Mart-2020] kwa lengo la kutangaza na kutafuta fursa mpya za soko la utalii nchini humo

Maonesho hayo maarufu na makubwa kabisa katika ukanda wa Asia-Pasifiki yalianza tarehe 03 Februari, 2020 na yamemalizika leo tarehe 05 Februari, 2020, Maonesho haya hufanyika kila mwaka katika Jiji la Mumbai na kushirikisha taasisi mbalimbali za utalii duniani.

Taasisi za Serikali zinazoshiriki ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Shirika la Ndege la Tanzania [Air Tanzania]. Kwa upande wa kampuni binafsi ni Zara Tours, Mount Meru Hotel na Nature’s Land Safaris & Rentals.

Katika Maonesho hayo, Banda la Tanzania limeibuka tena Mshindi wa Kwanza kwa upande wa Banda bora lilopambwa kwa unadhifu na kuvutia watu wengi [The winner of Best Decoration Award]. Tanzania imeshinda tunzo hiyo kwa mara ya pili mfululizo ambapo katika maonesho ya mwaka jana [2019], Tanzania pia ilishinda tuzo hiyo.

Balozi wa Tanzania nchini India Mhe. Baraka Luvanda amesema kuwa maonesho hayo ni fursa nyingine adhimu kwa nchi kutangaza vivutio vya utalii ambapo wafanyabiashara wapatao 15,000 wanaojishughulisha na masuala ya utalii walishiriki kutoka katika mataifa zaidi ya 50 duniani. Washiriki wamepata fursa ya kupeana taarifa muhimu kuhusu mwelekeo na maendeleo ya biashara ya utalii katika maeneo mbalimbali duniani, vivutio vipya pamoja na kufanya biashara.

Akiwa katika maonesho hayo, Balozi Luvanda alieleza kuwa maonesho yalisaidia washiriki wa Tanzania kukutana na wadau na kuanzisha uhusiano wa kibiashara unaotarajiwa kufungua soko la utalii nchini baada ya wadau hao kupata maelezo ya kutosha kuhusu vivutio vilivyopo nchini na faida zake. Kwa ujumla, India ina soko kubwa la utalii. Idadi ya watalii kutoka India wanaokwenda Tanzania sasa imeongezeka mara dufu baada ya kuanza kwa safari za ndege za Shirika la Ndege la Tanzania [Air Tanzania] moja kwa moja kutoka Tanzania kuja India na katika hilo alitoa wito kwa wafanyabiashara hao kuendelea kutumia fursa hiyo kuongeza idadi ya  watalii  wa India kutembelea Tanzania.

‘Nachukua fursa hii kwa dhati kuwapongeza sana Maafisa wote walioshiriki katika Banda letu la Tanzania la Maonesho kwa kazi nzuri ya kutangaza vivutio vya utalii nchini iliyowezesha tupate ushindi mwingine katika maonesho haya kwa mara ya pili kwa upande wa Banda bora lilopambwa kwa unadhifu na kuvutia watu wengi [The winner of Best Decoration Award]”, alisema Balozi Luvanda.