Nasaha Kutoka kwa Baraka H. Luvanda, Balozi wa Tanzania Nchini India, Wakati wa Mahafali ya Wanafunzi na Wanachama wa Umoja wa Wanafunzi wa Kitanzania Walioko Bangalore (Tanzania Students Association at Bangalore - TABASA), RG Royal Hotel, Bangalore.
Ndugu Yussuph Said,
Rais wa TASABA na Mwenyeji wetu,
Ndugu Bosco Kaweesi,
Rais wa 'Pan-African Federation and Students' Union', India,
Ndugu Nurat Ndyetabura,
Rais, Chama cha Wanafunzi wa Kitanzania-Acharya (TASAA),
Ndugu Viongozi Wengine katika Meza Kuu,
Ndugu Wageni Waalikwa,
Marafiki wa TASABA na TASAA,
Ndugu Wahitimu,
Mabibi na Mabwana,
Namaskar,
Asalaam Aleykhum,
Bwana Asifiwe,
Tumsifu Yesu Kristo.
Ndugu Rais,
Naomba nianze kwa kutoa shukrani nyingi kwa kunialika katika shughuli yenu ya mahafali leo hii. Nitamke wazi kuwa nimefurahia kukutanishwa nanyi, tena kwa idadi kubwa kiasi hiki na pia nimefurahi sana kusikia idadi kubwa ya wenzenu wameweza kutimiza lengo mahsusi lilowaleta nchini India.
Najua si rahisi hivyo kwani katika safari hiyo ngumu yalijitokeza magumu na vishawishi vya hapa na pale vilivyoweza kuwaathiri wengine wengi miongoni mwenu.
Aidha, niwashukuru uongozi wa TASABA na TASAA kwa mipango ya kilojistiki – malazi, mapokezi na mengineyo yote. Ukizingatia kuwa tulikuwa na heka heka za kuandaa hafla ya kusherehekea miaka 55 ya Muungano ambapo tumehitimisha jana tu isngekuwa rahisi kwetu kumudu mipango yote ya huku bila usaidizi wenu. Tunawashukuruni sana.
Ndugu Rais,
Ndugu Washiriki,
Niendelee na shukrani zangu kwa kwa kukupongezeni sana viongozi wa TASABA na TASAA kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha mnashughulikia changamoto nyingi zinazojitokeza katika eneo hili na maeneo jirani, tena kwa wakati na wakati mwingine bila hata kuhitaji msaada wa ubalozi. Kwa kazi hiyo nzuri, nawapongeza sana na kuwatia shime wale watakaokuwa wakipokea nyadhifa hizo siku zijazo kuendeleza kazi hiyo nzuri na ya mfano.
Ndugu Rais,
Ndugu Wahitimu,
Ndugu Waalikwa,
Mahafali ni tukio la kipekeee sana popote pale. Kwenu ninyi mliohitimu, tukio hili ni muda mahsusi wa kusherehekea, ni muda wa kutathmini mafanikio ya masaa mengi mliyotumia katika kuhakikisha mnafikia malengo yenu. Lakini pia siku kama ya leo mara sherehe hizi zinapohitimishwa ni muda wenu wa kutafakari ukurasa mpya wa maisha. Mlango wa dunia unafunguka na furaha, maumivu na wajibu mpya vinajitokeza. Nayasema haya si kwa kuwaogopesha, bali hiyo ndiyo hali halisi inayowakabili.
Ndugu Rais,
Ndugu Wahitimu
Mabibi na Mabwana,
Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa Tanzania kila mwaka inazalisha wahitimu wapatao laki nane na wote hao wanaingia katika soko la ajira. Changamoto kubwa iliyopo ni ufinyu wa ajira zenyewe, hususan katika sekta ya umma.
Pengine mtakuwa mmesikia kuwa Awamu ya Tano ya Uongozi ilikuwa imezuia kwa muda zoezi la kuajiri baada ya kuingia madarakani ili kuweza kushughulikia tatizo kubwa la watumishi hewa. Hivyo, mtakapofika huko mtakumbana na mrundikano wa wahitimu wenzenu waliokuwa wakisubiri kufunguliwa kwa ajira hizo na mtalazimika kupambana kweli kweli.
Lakini sitashangaa kusikia wengi miongoni mwenu mkifanikiwa kupata ajira serikalini na katika sekta binafsi na hata kujiajiri. Hii ni kutokana na elimu bora milyobahatika kuipata huku India inayosisitiza siyo tu elimu, bali pia stadi za maarifa (skills development). Ninawahimiza muende mkaoneshe maarifa hayo kwa vitendo na siyo kukaa na kulalamikia ufinyu wa ajira.
Ndugu Rais,
Wageni Waalikwa,
Niruhusu pia nitumie fursa hii kuwapongeza makundi mengine muhimu yaliyoshiriki kwa namna moja ama nyingine katika kufanikisha safari ndefu na ngumu ya wahitimu wetu hawa. Ninawapongeza sana wakufunzi wenu kwa kazi hiyo nzuri waliyoitekeleza kwa ufanisi mkubwa.
Pili, ni wazazi na walezi wa wahitimu hawa. Wazazi na walezi wameshiriki sehemu kubwa katika kuhakikisha mazingira rafiki yanakuwepo wakati wote wa safari ya masomo ya wahitimu wetu hawa. Wakati mwingine wazazi na walezi hawa walilazimika hata kwenda kukopa benki, au kwa ndugu na marafiki au hata kuuza chochote kilichowezekana ilimradi tu safari iendelee. Niwaombe tuwapongeze wakufunzi, wazazi na walezi hao kwa makofi mengi na mazito.
Ndugu Rais,
Wageni Waalikwa,
Ndugu Wahitimu,
Matarajio ya wazazi na walezi wenu baada ya kazi hii nzuri waliyoifanya ni makubwa. Matarajio ya wadogo zenu pia ni makubwa. Lakini pia matarajio ya nchi ni makubwa. Aidha, matarajio ya ndugu, hata wale wa mbali pia ni makubwa. Na kama ilivyokwishawahi kusemwa,ninanukuu: "Our prime purpose in life is to help others. And if you can’t help them, at least don’t hurt them." Nikiwaangalia nyuso zenu sioni hata mmoja wa kumuumiza mtu aliyechangia kumfikisha hapa siku ya leo.
Ndugu Rais,
Mabibi na Mabwana,
Katika kuhitimisha nasaha zangu, ningependa kutoa rai niliyowahi kuitoa mahali pengine. Mmehitimu ngazi hii ya elimu na katika fani mbali mbali hii. Sote tumejumuika hapa kukupongezeni sana. Lakini ninashawishika kuamini kuwa wengi wenu bado mna hamu na uwezo wa kujiendeleza zaidi ya hapo.
Hivyo, nawasihi pale ambapo fursa ya kujiendeleza zaidi itajitokeza ichangamkieni bila kusita. Kwani ni ukweli usiofichika kuwa when you buy a car or a piece of equipment it comes with a user’s manual with maintenance instructions. You have to service it regularly to ensure it continues to serve you well. How much more important is it to regularly service your brain after graduation? I know there are graduates who find no time to read a book again after graduation. Don’t be like that. For, a mind is like a garden. If it is not watered, and cultivated, weeds will take over.
Na nyongeza yenye maudhui kama hayo ni ile busara iliyomo kwenye maneno ya Henry Ford, ninanukuu: "Anyone who stops learning is old, whether at 20 or 80. Anyone who keeps learning stays young. Hence, the greatest thing in life is to keep your mind young."(mwisho wa kunukuu).
Nihitimishe kwa mchapo au hadithi fupi, lakini ya ukweli, yaani (anecdote). "Marafiki wawili walikuwa wakimzungumzia rafiki yao. "Sitamualika kamwe katika shughuli zangu, "mmoja alisema. "Mara ya mwisho alinifanyia kitu ambacho sikukipenda." "Ni nini alikufanyia?" " Si alikuja!"
Mlitualika nasi tukaitikia. Matarajio yetu ni kuwa mlimaanisha. Na tunaamini hatujafanya kitu chochote tofauti cha kusababisha kunyimwa mwaliko mwingine siku zijazo.
Baada ya kusema haya machache, nawashukuruni sana kwa kunialika na kama nilivyosema katika mchapo, ninaamini huu ni mwanzo tu wa mialiko mingine mingi siku zijazo.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.




