Dar es Salaam, 5 Disemba 2019 - Leo tarehe 5 Disemba 2019 Mhe. Innocent Bashungwa Waziri wa Viwanda na Biashara amefungua rasmi kongamano la biashara kati ya India na Tanzania katika ukumbi wa Kivukoni, Hoteli ya Serena Jijini Dar es salaam. Wakati akifungua kongamano hilo Mhe. Waziri Bashungwa amewataka wawekezaji kutoka India kuja kuwekeza katika viwanda vya nguo, ngozi, mafuta pamoja na kilimo kwa ujumla. Pia ameeleza kuwa kwa sasa serikali inashirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha Taifa linafikia malengo yake ya uchumi wa viwanda na wa kati ifikapo 2025.
Aidha, ameipongeza Shirikisho la Viwanda la India [Confederation of Indian Industry-CII] kwa kushirikiana na Ubalozi wa India hapa nchini kwa kuandaa kongamano hilo ambalo linalenga kuibua fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na India. Awali ufunguzi huo ulitanguliwa na hotuba fupi kutoka taasisi ya TPSF, CTI pamoja na CII ambao pia walihimiza uibuaji wa fursa za uwekezaji na ushirikiano wa kibiashara.
Mwisho wakati wa kongamano hilo wajumbe walishuhudia mabadilishano ya mikataba iliyosainiwa kabla ya kongamano hilo kati ya CII na TPSF pamoja CII na SADC Business Council ambayo inalenga kukuza ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji.