Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda akihutubia wakati wa Kongamano la kuvutia Biashara, Uwekezaji na Utalii lilifanyika katika hoteli ya Westin Jijini Chennai katika Jimbo la Tamil Nadu tarehe 05 Septemba, 2019. Kongamano hilo limeandaliwa na Shirikisho la Viwanda nchini India [Confederation of Indian Industry [CII] ambapo jumla ya wafanyabiasha 110 walihudhuria.

Wakati wa Kongamano hilo, pamoja na mambo mengine, Mhe. Balozi Luvanda alieleza kuwa Tanzania imefanya mabadiliko makubwa katika sera zake za kuvutia biashara na uwekezaji hususan, katika sekta ya viwanda ambapo alieleza kuwa, kwa sasa Tanzania kuna mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji ikiwa ni juhudi za serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kupitia Wizara na taasisi za Serikali kusikiliza na kutatua changamoto za wawekezaji na wafanyabiashara wa Ndani na Nje. 

Aidha, Mhe. Balozi Luvanda pia amewaomba wafanyabiasha hao kuongeza ushirikiano na Tanzania katika utalii, hasa ikizingatiwa kuwa India inatoa watalii zaidi ya Milioni 20 kwa mwaka kutembelea nchi mbalimbali duniani ikilinganishwa na Watalii Milioni 1.5 wanaoingia nchini Tanzania kwa mwaka, na katika hilo ametoa wito kwa wafanyabiashara hao kutumia fursa ya kuanza safari za moja kwa moja za ndege za Shirika la Ndege la “Air Tanzania” kutoka Dar es Salaam kuja Mumbai kuongeza idadi ya  watalii  wa India kutembelea Tanzania na kwa wawekezaji wake kwenda kuwekeza katika hoteli na fukwe za Tanzania.

  • Sehemu ya wafanyabiashara waliohudhuria kwenye Kongamano la kuvutia biashara, Uwekezaji na Utalii wakimsikiliza Balozi Luvanda [hayupo pichani].