New Delhi, 02 Novemba 2019
Tarehe 02 Novemba 2019 Mabalozi wa Nchi za SADC waliopo New Delhi walikutana katika hafla ya Siku ya SADC [SADC Day]. Hafla hiyo ilifanyika nyumbani kwa Balozi wa Tanzania nchini India ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kundi hilo lenye jumla ya nchi 15. Hafla hiyo ilihusisha Mabalozi wa Nchi za SADC nchini India pamoja na maafisa katika balozi hizo pamoja na wageni waalikwa kutoka katika Wizara ya Mambo ya Nje ya India.
Mgeni rasmi katika halfa hiyo alikuwa Mkurugenzi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya India, Sehemu ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bwana Rajesh Swami.
Balozi Luvanda alitumia fursa hiyo kuelezea pamoja na mambo mengine, suala la kuondolewa vikwazo nchini Zimbabwe. Alieleza kuwa Tamko dhidi ya vikwazo hivyo liliwasilishwa rasmi kwenye Mamlaka za Serikali ya India siku ya tarehe 25 Oktoba 2019 siku ambayo iliamuliwa na Viongozi Wakuu wa Nchi za SADC kuwa siku maalum ya kupaza sauti dhidi ya vikwazo hivyo.
Kwa upande wake, Mgeni rasmi katika shughuli hiyo, Mkurugenzi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya India, Sehemu ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, Bwana Rajesh Swami alieleza kuwa kwa miaka mingi uhusiano baina ya India na nchi za SADC umekuwa mzuri na kuwezesha biashara, uwekezaji, utalii, elimu, afya na uhusiano wa mtu na mtu kuimarika kwa kiwango cha juu.
Akihutubia katika hafla hiyo, Mgeni Maalum [Special Guest] Mhe. Fortune Chasi, Waziri wa Nishati wa Zimbabwe, alimshukuru Balozi Luvanda, Mwenyekiti wa Mabalozi wa Nchi za SADC nchini India na Mabalozi wote wa nchi za SADC nchini India kwa kuandaa hafla hiyo na jinsi walivyosimamia suala la kupaza sauti kupinga vikwazo dhidi ya nchi yake na kuwaomba waendelee na juhudi hizo hadi vikwazo hivyo vitakapoondolewa nchini Zimbabwe.