Utaratibu Unaotumika na Serikali Kugharamia Matibabu ya Wagonjwa Nje ya Nchi.

Serikali ina utaratibu wa kupeleka na kugharamia matibabu ya wagonjwa nje ya nchi, kwa wagonjwa ambao uchunguzi au matibabu yao, hayawezi kufanyika katika hospitali maalumu na za Rufaa  nchini kwa sababu ya kukosa vifaa tiba, wataalamu, na baadhi ya madawa ambayo hata kama madawa hayo yangekuwepo nchini bado isingekuwa rahisi kutumika kwa kuwa, hakuna huduma ya maabara kwa ajili ya kupima viwango vya madawa hayo mwilini na urekebishwaji wake.

Wagonjwa hao ni lazima wapendekezwe na jopo la Madaktari Bingwa, sio chini ya watatu, na kupitiwa na Wakurugenzi watendaji, kutoka katika hospitali maalum za Rufaa nchini. Kisha ombi la rufaa litapelekwa Wizara ya Afya na Ustawi Wa Jamii ili kujadiriwa katika Kamati kwa ajili ya kupata kibali cha kutibiwa nje ya nchi.

Baada ya rufaa kupata kibali cha Kamati, mgonjwa ataandaliwa na kupelekwa nje ya nchi, ili kupatiwa huduma ya matibabu, kwa gharama za serikali. Fursa hii ipo sawa kwa wananchi wote.

Utaratibu huu ni maalum kwa ajili ya kuandaa rufaa ya namna hiyo na hatimaye kupata Kibali cha Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii. Hospitali husika zinazotoa rufaa ni Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (Jakaya Kikwete Cardiac Institute)Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI), Taasisi ya saratani ya Ocean Road (ORCI) za Dar es Salaam, Hospitali ya Rufaa ya Mbeya (MRH), Hospitali ya KCMC, Kilimanjaro na Hospitali ya Bugando, Mwanza, ambazo zinaufahamu na kuutumi utaratibu huo.

Changamoto

Hata hivyo, kuna baadhi ya Madaktari katika hospitali hizo, ambao hawazisimamii taratibu zilizowekwa na Serikali.  Aidha baadhi ya wagonjwa husafiri kwenda nje, bila kupata rufaa na ushauri maalumu. Hali hiyo, huwaletea usumbufu wagonjwa wengi na hospitali za nje zinazowapokea na Serikali kwa ujumla, hasa pale ambapo gharama za matibabu zinapokuwa juu, kuliko uwezo wa mgonjwa alivyojiandaa.

Kwa kuzingatia hali hii, Wizara inatoa tahadhari, kwa wale wote wanaokwenda kupata matibabu nchi za nje, bila kufuata utaratibu uliowekwa, kwamba, Serikali haitahusika na gharama za mgonjwa atakayetafuta matibabu nje ya nchi, kinyume na utaratibu uliowekwa.

Iwapo utaratibu uliowekwa wa rufaa haukufuatwa, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii haitakubaliwa kisheria, kugharamia huduma zote, za uchunguzi au matibabu yatakayotolewa na hospitali za nje ya Tanzania. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inawaomba wananchi wanaokuja nchini India kwa matibabu ya kujigharamia wenyewe ni vema wapate maelezo ya kina kuhusu matibabu yao kabla ya kuondoka nchini kuja India katika Wizara ya Afya-Kitengo cha Wagonjwa wa Nje ya Nchi au Ofisi ya Mwambata wa Afya, Ubalozi wa Tanzania, New Delhi kwa barua pepe: kheri.goloka@nje.go.tz.

Tunaomba tushirikiane ili kuepusha matatizo.