Ujumbe wa Maafisa wawili kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania [Tanzania Revenue Authority – TRA] Bw. Nassor U. Siriwa na  Bw. Narcis A. Lumumba pamoja na mwakilishi wa sekta binafsi, Bw. Clement S. Munisi kutoka Jumuiya ya Viwanda Tanzania   [Confederation of Tanzania Industries - CTI] waliwasili New Delhi, India tarehe 29 Julai, 2012 kwa ziara ya kikazi ya siku tano.

Madhumuni ya ziara ya Ujumbe huo ni kuja kukutana na Mamlaka za kodi/ushuru za Serikali ya India ili kupata taarifa sahihi  za mfumo wa kodi/ ushuru kwa bidhaa za nguo zinazotoka India.

Baada ya maamkizi, Kiongozi wa Ujumbe Bw. Nassor Siriwa alikiarifu Kikao kwamba, ziara yao imefuatia malalamiko ya muda mrefu ya wenye viwanda vya nguo pamoja na wadau wa sekta hiyo Tanzania  kuhusu  bidhaa za nguo [textile] zinazoingizwa nchini kutoka India, Pakistan na China kuwa rahisi mno kiasi cha kuvuruga soko la bidhaa za nguo zinazotengenezwa na Viwanda vya Tanzania na hata zile zinaoagizwa kutoka nchi nyingine duniani.

Alisema suala hilo vile vile lilishasemewa na Waziri wa Viwanda ambaye alisema kuwa kuingizwa nchini bidhaa hizo za nguo rahisi kutoka India, Pakistan na China  kunaleta ushindani wa kibiashara usiokuwa wa haki [unfair competition] na vile vile kunauwa viwanda vya nguo vya Tanzania. 

Alisema Wadau wa sekta ya nguo, walitoa mapendekezo mbali mbali kuhusu hatua za kurekebisha au kumaliza kabisa tatizo hilo, zikiwemo  hatua ya kupanga ushuru maalum [specific tariff] kwa bidhaa za nguo zinazotoka India, Pakistan na China pamoja na hatua ya kupiga marufuku kabisa uingizaji wa bidhaa za nguo kutoka katika nchi hizo. 

Imefahamika kwamba kwa mujibu wa makubaliano ya Ushuru wa Forodha [Common External Tariff – CET] ya Jumuiya ya Afrika Mashariki [East African Community – EAC] ya mwaka 2005, pamoja na sheria zinazoratibu ushirikiano wa kibiashara za Shirika la Biashara Duniani [World Trade Organisation – WTO], Mamlaka ya Mapato Tanzania haiwezi kuchukua hatua hizo  zilizopendekezwa na wadau.

Kwa Taasisi hiyo kuchukua hatua dhidi ya waagizaji/uagizaji  wa bidhaa hizo haina budi kwanza kuwa na ushahidi [substantive evidence] wa kutosha utakaothibitisha wazi ukiukwaji wa taratibu za kodi/ushuru kwa bidhaa husika katika nchi zinakotoka. Na kwa misingi hiyo, kiongozi wa Ujumbe huo alieleza kuwa Kamishna Mkuu wa TRA amewaagiza kuja kuonana na Maafisa wa Serikali za nchi kusika  ikiwemo India na China, ili kupata uhakikika/uhalisia wa suala hilo kwa lengo la kulitolea maelezo/maamuzi muafaka.

Ujumbe huo wa TRA ambao ulianzia ziara yake nchini China, ambako walionana Maafisa wa Serikali ya nchi hiyo, umesema,  wanachotegemea  kutoka katika Serikali ya India ni kupatiwa taarifa/ takwimu sahihi za taratibu za utozaji wa ushuru wa forodha kwa wasafirishaji/wauzaji [Exporters] wa bidhaa za nguo, taarifa ambazo zitatumika kulinganisha na kutathmini  pamoja na kufikia maamuzi muafaka ya tatizo hilo.

Naye Kaimu Balozi, Bi Badriya Kiondo, aliwaarifu Maafisa hao wa TRA kwamba, baada ya juhudi kubwa Ubalozi  umefanikiwa  kuwapatia miadi ya kuonana na Maafisa wa Kitengo cha Forodha wa Wizara ya Fedha ya Serikali ya India.

Alisema tatizo hasa lililochelewesha kupatikana kwa miadi hiyo ni kwamba Tanzania na India hazina makubalino [Bilateral agreement] ya ushirikiano wa masuala ya forodha, hivyo iliwawia vigumu Maafisa wa Serikali ya India kukubali kuwa na mazungumzo na Maafisa wa TRA kazungumzia masuala ya ushuru.

Aidha, Kaimu Balozi, aliwanasihi Maafisa hao wa TRA kuitumia vyema fursa hiyo waliopata ili kufanikisha jukumu walilopewa na Serikali.

Vile vile, aliwaeleza kwamba Wizara ya Fedha ya India imewaruhusu [ikiwa wataafiki] kuhudhuria mafunzo maalum kuhusu masuala ya ushuru wa forodha ambayo yanafanyika huko Faridabad nje kidogo ya mji wa Delhi.

Pamoja na nasaha hizo Maafisa hao wa Mamlaka ya Mapato Tanzania walikubaliana na ushauri waliopewa na Kaimu Balozi wa kutembelea baadhi ya viwanda vya nguo vilivyopo Delhi, ili kupata mwanga wa bei halisi za bidhaa hizo za nguo viwandani, ambako wafanyabiashara ndiko wanakonunua.

Kwa kumalizia Ujumbe huo ulimshukuru Kaimu Balozi pamoja na Maafisa wote wa Ubalozi kwa ushirikiano mkubwa waliowapa katika kufanikisha utekelezaji wa  jukumu hilo la taifa.

Aidha, walikiri kwamba ilivyokuwa ushrikiano wa kiuchumi, biashara nk. baina ya Tanzania na India unaendelea kukua, ipo haja kwa nchi hizi mbili  kuwa na makubaliano ya ushirikiano wa masuala ya forodha ili kuepusha matatizo kama haya katika siku za usoni.  Maafisa hao wamehidi kufikisha taarifa hizo katika ngazi husika kwa maelekezo zaidi.

Ujumbe huo wa TRA uliondoka Delhi tarehe 3 usiku kurejea nyumbani.