New Delhi-Julai 20, 2022-Ubalozi wa Tanzania, New Delhi umeratibu na kushiriki kikamilifu katika Kongamano la Kimataifa la kibisahara na Uwekezaji kati ya India na Afrika “17th CII EXIM Bank Digital Conclave on India-Africa Project Partnership” lililofanyika katika hoteli ya Taj Palace, jijini New Delhi kuanzia tarehe 19-20 Julai 2022. Kongamano hilo liliandaliwa na Shirikisho la Viwanda nchini India (Confederation of Indian Industry-CII) wakishirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje ya India na hufanyika kila mwaka. Kauli-Mbiu ya Kongamano la mwaka huu ni “Creating Shared Futures”. Aidha, Kongamano hili lilikuwa na agenda mbalimbali ambapo agenda kuu zilihusu uhimizaji wa maendeleo ya biashara na uwezekaji kati ya India na Afrika. Masuala mengine yalikuwa ni pamoja na usalama wa chakula na nishati hususan, katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na uhaba wa chakula na nishati kutokana na mgogoro wa Ukraine.
Kongamano la mwaka huu limefanyika mjini New Delhi kwa mara ya kwanza baada ya India kuondoa mazuio ya kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa UVIKO-19 yaliyokuwepo tangu mwaka 2020. Takriban wahiriki 2000 kutoka nchi 72 zikiwemo, nchi 45 za Afrika, Mawaziri 32 kutoka nchi 18 za Afrika na Mawaziri 3 wa India na Wawakilishi wa Makampuni ya Kihindi 600 walishiriki Kongamano hili. Aidha, Makamu wa Rais wa Mauritius, Mhe. Marie Cyril Eddy Boissezon, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Gambia, Mhe. Bandara A. Joof, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Zambia, Mhe. W. K. Mutale Nalumango na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwah walishiriki.
Katika Kongamano hilo masuala mbalimbali ya kuimarisha Biashara na Uwekezaji kati ya India na Afrika katika sekta za Nishati, Maji Kilimo, Uendelezaji wa Miundombinu, Huduma za Afya, Teknolojia ya Mawasiliano (ICT) na Ufadhili wa Miradi (Project financing) yalijadiliwa kwa kina. Kampuni za India na Serikali ya India zilionesha utayari wao kama mshirika thabiti wa maendeleo ya Afrika. Aidha, Makampuni hayo yalitoa fursa kadhaa za kisekta katika biashara na uwekezaji barani Afrika huku wakisisitiza umuhimu wa kuwepo mazingira bora ya uwekezaji. Kongamano hili liliwezesha majadiliano ya wazi na ufahamu kati ya wadau wakuu kutoka nchi za Afrika na India na kuongeza zaidi ushirikiano na mikakati thabiti ya kibiashara na uwekezaji hususan, katika kipindi hiki baada ya janga la UVIKO-19 kudhibitiwa.
Kongamano lilifunguliwa tarehe 19 Julai 2022 kwa hotuba ya kina ya Waziri wa Biashara na Viwanda wa India, Mhe. Piyush Goyal. Mawaziri wengine wa Serikali ya India walioshiriki katika Kongamano hili ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. S. Jaishankar na Mhe. V. Muraleedharan, Waziri wa Nchi anayeshughulika na Mambo ya Nje ya India ambaye alilifunga kongamano hilo tarehe 20 Julai 2022.
Ujumbe wa Tanzania katika kongamano hili uliongozwa na Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Uweso (Mb.) ambaye alitumia fursa ya Kongamano hilo muhimu kuwasiliana na wadau mbalimbali na kuelezea fursa mbali mbali za biashara na uwekezaji zilizopo Tanzania pamoja na kuwashawishi wawekezaji hao kuwekeza nchini Tanzania hususan, katika sekta ya miundombinu ya maji. Aidha, wakati wa hotuba yake, Waziri Mhe. Aweso alieleza kuwa ushirika wa Tanzania na India ni wa kimaendeleo ambapo Tanzania imekuwa ikifaidika na misaada mbalimbali ya kimaendeleo ikiwa ni pamoja na ufadhili katika kutekeleza miundombimu ya maji katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Kanda ya Ziwa pamoja na Zanzibar.
Kama ilivyokuwa mwaka jana (2021), kongamano la mwaka huu (2022) lilifanyika wakati biashara na uwekezaji duniani vimeendelea kuzorota kutokana na janga la UVIKO-19 pamoja madhara ya vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine. Takwimu zinaonesha kuwa thamani ya biashara kote duniani ilipungua kwa asilimia 9 (2020). Aidha, uwekezaji wa moja kwa moja (Foreign Direct Investment (FDI) duniani ulipungua kwa asilimia 42 katika kipindi cha mwaka 2020 ingawa uliongezeka hadi kufikia Dola za Kimarekani Trilioni 1.6 katika kipindi cha mwaka 2021 ambapo unategemea kupungua katika kipindi hiki cha mwaka 2022. India ikiwa mwenyeji wa mkutano huo, ilihimiza biashara na uwekezaji duniani kwa kushirikiana na nchi za Afrika ambapo India inashika nafasi ya tano (5) katika kufanya biashara na Afrika ambapo kwa takwimu za mwaka 2018-2019 thamani ya biashara kati ya India na Afrika ilikuwa Dola za Kimarekani Bilioni 69.7.
Aidha, India inashika nafasi ya tano (5) katika uwekezaji Afrika ambapo thamani ya uwekezaji wa India barani Afrika kwa sasa ni Dola za Kimarekani Bilioni 73.9. Vilevile, ukubwa wa biashara kati ya India na Afrika umekua na kufikia Dola za Kimarekani Bilioni 89.5 mafanikio hayo yamepatikana baada ya nchi 54 kati ya 55 za Afrika ikiwemo, Tanzania kujiunga katika Eneo Huru la Biashara la Afrika (African Continental Free Trade Area-AfCFTA) lenye watu takribani bilioni 1.2 pamoja na ukubwa wa pato la jumla (Collective GDP) la kiasi cha Dola za Kimarekani Trilioni 2.4. Vilevile, imeelezwa kuwa Mpango wa Msamaha wa Ushuru wa Bidhaa (Duty Free Tariff Preference (DFTP) Scheme) ulioanzishwa na India ambapo Tanzania ilijiunga rasmi mnamo tarehe 22 Mei 2009 umechochea kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa biashara ya mauzo ya bidhaa za Afrika nchini India ambapo kupitia mpango huo India inatoa msamaha wa ushuru hadi wa kiwango cha Asilimia 98.2 kwa mauzo ya bidhaa za Afrika zinazoingizwa nchini India.
Kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Mhe. Dkt. S. Jaishankar wakati wa hotuba yake kwenye kongamano hili tarehe 19 Julai, 2022, India imetoa mikopo ya masharti nafuu (LoC) ya kiasi cha Dola za Kimarekani Bilioni 12.3 kutekeleza Miradi mbalimbali barani Afrika. Miradi 197 imeshatekelezwa, miradi 65 inaendelea kutekelezwa na miradi mingine 81 hiko katika hatua za kuanza kutekelezwa. Tanzania ni mnufaika mmojawapo wa miradi hiyo, hususan miradi ya maji na TEHAMA.
Mbali na maonesho ya biashara ambayo kwa kawaida huenda sambamba na Kongamano hilo, mwaka huu CII pia ilipiga hatua ya ziada kwa kuendesha maonesho ya wazi ambapo wawakilishi wa Jumuiya za biashara za nchi za Afrika walipata fursa za kutangaza fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zilizopo katika nchi zao ambapo walipata nafasi na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na wafanyabiashara wa India. Kupitia banda la Tanzania la maonesho ya Biashara, Uwekezaji na Utalii katika kongamano hilo, Ubalozi kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) pamoja na ofisi ya uhamasishaji na uratibu wa biashara na uwekezaji (INDIA TANZANIA TRADE COMMISSION (ITTC) ya Chennai uliweza kutangaza fursa nyingi za biashara, uwekezaji na utalii zilizopo Tanzania.
Aidha, tarehe 20 Julai 2022, Waziri Mhe. Aweso alikutana na kufanya mazungumzo na Bibi Harsha Bangari, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Exim ya India. Katika kikao hicho Mhe. Waziri Aweso kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliishukuru Benki ya Exim ya India kwa kushirikiana na Tanzania hususan, katika sekta ya maji katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maji ikiwemo mradi mkubwa wa maji wa Shinyanga-Igunda Tabora na Tinde-Shelui.
Vilevile, alimshukuru Mkurugenzi huyo kwa kuendelea na ufadhili katika utekelezaji wa mradi wa kihistoria wa miji 28 ambapo benki hiyo imetoa zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 500. Kadharika, Waziri Aweso ameiomba Banki ya Exim ya India kuendelea kushirikiana na kuiunga mkono Tanzania kifedha katika kuendelea kutekeleza miradi ya maji ya kimkakati ambapo katika kusisitiza hilo, Waziri Aweso alitoa wasilisho lenye mapendekezo ya maeneo muhimu kwasasa huku akilenga na kusisitiza kwa pamoja kuendelea kudumisha ushirikiano baina ya Tanzania na India katika eneo muhimu la kuendeleza miundombinu ya maji.