New Delhi, Juni 12, 2020 - Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi tarehe 12  Juni, 2020 amempigia simu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ambapo, viongozi hao wamezungumzia masuala yahusuyo uhusiano na ushirikiano mzuri, wa kirafiki na kihistoria uliopo kati ya Tanzania na lndia.

Katika mazungumzo hayo Mhe. Modi amempogeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi wake wa Awamu ya Tano na amemtakia heri yeye na Watanzania wote katika juhudi kubwa za kuijenga nchi zinazoendele na Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

Pamoja na kumhakikishia kuwa India itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania katika nyanja mbalimbali hasa kiuchumi, Mhe. Modi amempa mrejesho wa yaliyojiri katika. mkutano wa nchi 20 tajiri duniani (G20), uliofanyika hivi karibuni ( India ikiwa ni mojawapo) ambapo nchi hizo zimekubaliana kuwa taasisi za fedha za kimataifa zitoe msamaha wa madeni kwa nchi masikini na zinazoendelea, zilizopata madhara kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19).

Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Modi kwa kumpigia simu, kumtakia heri na kumpa mrejesho wa yaliyojiri katika mkutano wa G20, na ameomba taasisi za fedha za kimataifa zitakapotoa msamaha wa madeni ziitupie macho Tanzania ambayo pia imepatwa na madhara ya ugonjvva wa Corona ili iweze kuimarisha uchumi wake.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza India kwa juhudi za kutafuta chanjo ya virusi ya Corona ambazo anaamini zitafanikiwa na kwamba Tanzania ikiwa moja ya nchi zilizokumbwa na ugonjwa huo itanufaika, japo ugonjwa wenyewe unapungua kwa kasi kubwa nchini Tanzania.

Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Modi kwa uhusiano na  ushirikiano mzuri wa Tanzania na India ambayo ni miongoni nchi 5 zinazoongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania na pia ameshukuru kwa mikopo nafuu inayotolewa na India kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa nchini Tanzania.

Ameitaja baadhi yake kuwa ni mkopo wa ujenzi wa Taasisi ya Teknolojia ya Nelson Mandela, mikopo ya miradi ya maji na ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa wanafunzi wa Tanzania wanaokuja kusomea masuala ya afya, uhandisi na TEHAMA nchini India.

Mikopo ya miradi ya maji ni pamoja na shilingi Bilioni 225.9 ( Ruvu - Dar es Salaam, ambao umekamilika), shilingi Bilioni 611.5 (Maji ya Ziwa Victoria kwenda Tabora, Nzega na Igunga ambao unakaribia kukamilika), shilingi Trilioni 1.2 (miradi ya maji ya Miji 28, ambapo utekelezaji wake unaendelea) na shilingi Bilioni 209.9 (miundombinu ya maji ya Zanzibar ambayo inaendelea kujengwa).

Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia Mhe. Modi kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na  ushirikiano  wake  na  India,  na  amewaalika wafanyabiashara na wawekezaji wa India kwenda Tanzania kuwekeza  katika sekta mbalimbali   zikiwemo viwanda,    kilimo,    ufugaji,    madini   na   nyingine   kwani Tanzania imejenga mazingira mazuri ya uwekezaji.