New Delhi, Juni 09, 2020 - Awali ya yote nachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema kwa kutukutanisha sote leo hii kwa njia hii ya mtandao. Pili, naomba niwashukuru Bodi ya Utalli kwa wazo hili zuri na pia kwa kuwezesha TEHAMA kufanikisha mkutano. Tatu, naomba niwashukuru maafisa wetu kwa maandalizi mazuri ya mkutano huu. Na mwisho lakini si kwa umuhimu, nawapongeza watoa mada waliotupitisha kwenye hali ya utalii nchini baada ya COVID-19. Nawshukuru pia Waheshimiwa Mabalozi, Dkt. Dau na Mbelwa Kairuki kwa kuwasilisha vema na kuifanya kazi yangu sasa kuwa nyepesi.

Ndugu Mwenyekiti,

Ndugu Wajumbe,

Eneo langu la uwakilishi ni pana sana, nalo linahusisha nchi nne zilizoko Kusini mwa Bara la Asia ikiwemo India, Nepal, Bangladesh na Sri Lanka pamoja na Singapore ambayo iko Kusini Mashariki mwa Bara la Asia. Na nyote mnafahamu kuwa India pekee ina jumla ya watu takriban Bilioni. 1.3; Bangladesh-Milioni 170; Nepal- Milioni 29,136,808; Sri Lanka-Milioni 21,413,249 na Singapore-Milioni 5,850,342..

Na ni kwa mantiki hiyo, kwa muda mchache niliopewa nitajielekeza zaidi kuzungumzia mustakabali wa India na kuacha nchi zingine kwa ajili ya mjadala utakaopangwa wakati mwingine.

SEKTA YA UTALII NCHINI INDIA (AN OVERVIEW)

Sekta ya utalii nchini India imekuwa ikichangia asilimia 9.2 (Bilioni 268.3 USD) katika Pato la Taifa la India na asilimia 5.4 ya fedha zote za kigeni. Mathalani, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020, yaani mwezi Aprili 2020,  sekta ya utalii iliingiza mapato ya nje (Forex) kiasi cha USD bilioni 29.962.

Aidha, shughuli za kiuchumi katika sekta ya utalii zinaajiri zaidi ya watu milioni 87 (12.75%) kwa mwaka. Vile vile, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 jumla ya watalii milioni 10.9 waliitembelea India. Kadhalika,wahindi milioni 26.3 walikwenda nje ya nchi kwa shughuli za utalii. Hadi kufikia mwezi Februari 2020 ni watalii 1.01 milioni walitembelea India. Sekta hii kama itakavyoelezwa baadaye, imeathiriwa zaidi kutokana na ukweli kwamba inategemea zaidi mapato ya watalii wanaotoka nje ya nchi ambao kwa sasa kutokana na ugonjwa huu, wameshindwa kusafiri na wengi wao wamesitisha safari za kuja India.

Kwa ujumla, India ina soko kubwa la utalii. Kwa kadri ya uchumi wa India unavyoongezeka ndivyo idadi ya watalii kutoka India kwenda nje  inazidi kuongezeka. Kwa mfano, mwaka 2018 wahindi 26 milioni walikwenda nje ya nchi kutalii  na kutumia dola za kimarekani takribani Bilioni 25.4. Kwa kawaida Mtalii kutoka India hutumia wastani wa dola za kimarekani 1,200 kwa safari moja na ilikadiriwa hadi kufikia mwisho wa  mwaka wa fedha 2020/2021, yaani mwezi Aprili 2021, wahindi milioni 50 wangekuwa wamesafiri kwenda nje ya nchi kutalii.

Kwa upande wa Tanzania, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015 takribani watalii elfu  50,000 kila mwaka kutoka India, idadi ambayo ni mara dufu ya  idadi iliyokuwepo miaka kadhaa kabla ya mwaka 2015. Ongezeko hili limechagizwa kwa kiasi kikubwa, hatua madhubuti za kujitangaza ikiwemo, hatua ya Serikali ya kurejesha usafiri wa ndege wa moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Mumbai kwa kutumia ‘Air Tanzania” tangu mwezi Julai 2019.

ATHARI ZA COVID-19 KATIKA SEKTA YA UTALII

Kama ilivyo katika nchi nyingine, sekta ya utalii nchini India imeathirika sana kutokana na  na janga la ugonjwa huu hususan,  kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na nchi nyingi, ikiwa ni pamoja na  India yenyewe kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.

Katika kukabiliana na janga hili, mataifa ambayo ni masoko muhimu ya utalii nchini India, kama vile mabara ya Ulaya, Amerika na Asia yalichukua hatua mbalimbali za kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo. Hatua hizo zilijumuisha kuzuia raia wake kusafiri na baadhi ya mashirika ya ndege kutofanya safari nje ya nchi, hali iliyosababisha kuathirika kwa sekta hiyo. Aidha, ugonjwa huu umeleta athari kubwa kwenye sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Tarehe 22 Machi 2020, India ilichukua hatua ya kufunga na kudhibiti mipaka yake, amri ya kuzuia watu kutotoka majumbani mwao (lockdown) na kusimamisha watu kutoa huduma mbalimbali isipokuwa kwa wale wanaotoa huduma muhimu tu kwa jamii pamoja na kutoa zuio la kuingia na kutoka kwa ndege za Kimataifa pamoja na vyombo vingine vya usafiri majini kama vile meli (Cruise ships) na reli. Hatua zote hizi zimesababisha madhara makubwa katika sekta ya utalii nchini India.

Baada ya janga la COVID-19 kuingia, Serikali ya India ilifanya tathmini na kubaini kuwa madhara makubwa ya ugonjwa huu katika sekta ya utalii yalianza kujitokeza  mwanzoni mwa mwezi  Machi, 2020 tofauti na miezi ya Februari na Januari, 2020 ambapo hali bado ilikuwa shwari.

Kutokana na janga hili, sekta ya Utalii nchini India inategemea kukosa mapato kupata hasara ya zaidi ya Rupees trilioni  5-10 sawa na USD 67-135 Bilioni katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 kutokana na kufungwa kwa hoteli pamoja na kusimama kwa huduma za usafiri wa anga ambayo ni asilimia 70 ya mapato ya mwaka 2019. Katika kipindi cha kuanzia mwezi Aprili-Juni 2020, sekta ya utalii imepoteza mapato ya kiasi cha Rupees Crores 69,400 (USD Bilioni 9).

Aidha, inasemekana watu zaidi ya milioni 38 wamepoteza ajira katika sekta hii. Vile vile, sekta ya usafiri wa anga nchini India inategemewa kupata hasara ya kiasi cha dola za kimarekani Bilioni 3.3-3.6 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha, Aprili-Juni- 2020.

HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI YA INDIA

Hatua kadhaa zimechukuliwa na Serikali ya India zikilenga, pamoja na mambo mengine, kudhibiti janga hili na wakati huo kuwezesha maisha ya watu wake hususan, wa hali ya chini kupata mahitaji ya lazima kama vile chakula na matibabu. Aidha, sekta binafsi na watu binafsi wamejitolea sana katika kuongezea uwezo mfuko wa majanga.

Ni kwa mnasaba huo, Serikali imeidhinisha matumizi ya fedha kwa ajili ya kuvinusuru Viwanda Vidogo Vidogo na vya Kati (MSMEs) kiasi cha Rupees Crores laki tatu (sawa na dola za kimarekani  Bilioni 40.5),  ambapo sekta ya utalii imeomba kupatiwa kiasi cha  dola za marekani Bilioni 6.8 ili kusaidia kurejesha uwezo wa sekta hii muhimu kuhimili hali ya mdodoro wa uchumi baada ya COVID-19.

Aidha, Serikali ya India, kwa makusudi na kwa kuzingatia kuwa janga la COVID-19 ni la muda mrefu, imechukua hatua za kurejesha shughuli muhimu za ujenzi wa uchumi na uzalishaji ili kukabiliana na hali inayojulikana kama ‘pent up demand’, ambayo ni hali ya uhitaji mkubwa wa bidhaa na huduma kutokana na shughuli za uzalishaji kusitishwa mnamo mwezi Machi mwaka huu.

Ni matarajio kuwa wakati wowote sasa, India itafungua shughuli zote za kiuzalishaji na huduma katika hali ya kawaida licha ya kuwa maambukizi bado yapo.

NINI KIFANYIKE BAADA YA HALI KUWA HIVI ILIVYO

COVID-19 ni janga ambalo limeikumba dunia na halioneshi dalili yoyote ya kuwa litakwisha hivi karibuni. Kwa mfano, pamoja na India kuchukua hatua kali katika kudhibiti milipuko ya ugonjwa huu, bado kufikia leo tarehe 9 Juni 2020 ina jumla ya visa 266,598;vifo 7,466 na waliopona 129,214. Hali katika maeneo mengine ya jirani inaendelea kuwa tete licha ya hatua za udhibiti wa ugonjwa huu.

Hivyo basi, ni muhimu na sharti mikakati na mbinu mpya za kuvutia watalii zibadilike kuendana na nyakati zilizopo:

Ni maoni na ushauri wetu kuwa, Wizara ya Utalii sasa itumie zaidi njia za kielekitroniki/kidijitali, ikiwemo; mitandao ya kijamii kwa ajili ya  kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii ili kuhamasisha watalii kutembelea nchini baada ya COVID-19 kudhibitiwa. Hata hivyo, tunashuari kuwa taarifa za mitandao hiyo ya kijamii zihakikiwe kabla ya kuchapishwa ili kutoa taarifa sahihi kwa wadau mahsusi na pia zizingatie tamaduni, imani na mila za maeneo husika. Kwa mfano, wakati mwingine imejitokeza taarifa zinazohusu ulaji wa nyama ya ng’ombe kutangazwa kwenye eneo hili la uwakilishi ambapo si sahihi.

Aidha, pamoja na kuendelea kuhamasisha wadau kuhusu matumizi ya utambulisho mpya wa utalii Tanzania (Tanzania Unforgettable), ni maoni na ushauri wetu kuwa utambulisho huo utengenezewe tovuti mahsusi (https://Tanzania Unforgettable.go.tz) kama iliyo hapa India “Incredible India” ambapo taarifa zote muhimu kuhusu vivutio vya utalii, aina ya mazao ya Utalii, vitapatikana kwenye tovuti hiyo ili iwe rahisi kwa watalii walioko sehemu mbalimbali duniani kujua vivutio vilivyopo nchini.

Vile vile, kwa hali ilivyo sasa ni vigumu kuandaa mikutano, makongamano na kushiriki katika maonesho mbalimbali ya kutanganza utalii nje ya nchi. Hivyo, ili kurahisisha shughuli za kujitangaza, tunashauri kuwepo na Mobile App ya Tanzania Unforgetable (Tanzania Unforgettable App.) ili taarifa kuhusu vivutio vya utalii nchini ziwafikie watu wengi zaidi na katika sehemu mbalimbali duniani kwa urahisi.

Kadhalika, ni maoni na ushauri wetu kuwa upo umuhimu wa kuhamasisha zaidi raia wa kigeni na diaspora kama vile, Muingereza anayejitambulisha kwa jina “Boli Zozo” ambaye anafanya kazi nzuri ya kuitangaza Tanzania. Wengine ni kama vile  wacheza filamu na watengenezaji wa filamu maarufu wa India (Bolywood) ambao kwa bahati nzuri Bodi ya Utalii imekwsihaona umuhimu wao na tayari inashirikiana nao. Wote hawa wangepaswa kutambuliwa umuhimu wao na kuwahamasisha wafanye zaidi kwa kuwatunuku tuzo za utalii zinazolenga kuwatambua na kuwapa hamasa ya kufanya kampeni hizo zaidi.

Pia, kutokana na uzoefu wa India wa “wellness Tourism”, ambapo wanatumia tiba asili na yoga katika kuvutia watalii wengi sana. Uzoefu kama huo ungeweza kutumika hata sasa tunapoendelea kuhamasisha watanzania kutumia njia ya kujifukiza (nyungu) katika kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19.

HITIMISHO

Tunapongeza na kuunga mkono jitihada kubwa zilizochukuliwa na Serikali katika kudhibiti ugonjwa wa COVID-19 na kutoa kipaumbele katika kuepusha taharuki kwa jamii ya watanzania. Hatua hii imeliweka Taifa kuaminika zaidi na watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani na kuwezesha wengine kuanza kuitembelea nchi yetu.

Aidha, tunapongeza utayari uliopo nchini wa kuanza kupokea watalii baada ya kufungua shughuli za kiuchumi hususan, katika viwanja vyetu vya Kimataifa vya ndege pamoja na Shirika la Ndege la Tanzania ambalo limeonesha uwezo, weledi mkubwa na utayari wa kufanya kazi katika mazingira ya COVID-19, ambapo wamefanikisha kuwarejesha nchini watanzania waptao 438 kutoka India na kuwarejesha kutoka Tanzania raia 202 wa India waliokuwa wamekwama nchini Tanzania. Kwa taarifa tu, tunakamilisha mpango wa awamu ya 3 ya safari hizi.

Vile vile, tunapongeza sana uamuzi wa Serikali kuondoa suala la karantini ya lazima ya siku 14 kwa wageni waliokuwa wanaingia nchini kwani Karantini ni sababu tosha ya mtalii kusita kufanya safari yake.

Mwisho, tunashauri katika mikutano ya aina hii ni vizuri kushirikisha uongozi wa ATCL ili watoe mipango yao inayorandana na mikakati ya kukuza utalii. Upo umuhimu kwa Air Tanzania kuanza kujipenyeza kila mahali hususan, kwenye maeneo ya kimkakati kama vile China, Japan, Singapore, Indonesia, Malaysia na Korea Kusini.