New Delhi, Julai 07, 2022 - Ubalozi wa Tanzania nchini India kwa kushirikiana na diaspora wa Tanzania nchini India uliandaa na kuratibu hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika katika makazi ya Balozi jijini New Delhi tarehe 07 Julai 2022. 

Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 23 Novemba 2021 Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) katika Mkutano wake wa 41 wa nchi wanachama wa shirika hilo uliofanyika katika Jiji la Paris nchini Ufaransa lilitangaza kuwa tarehe 07 Julai ya kila mwaka itakuwa ni Siku ya Kiswahili Duniani.

Maadhimisho hayo yalipambwa na shughuli mbalimbali zikiwemo: Maonesho ya mavazi ya mwafrika, uimbaji wa nyimbo za kiswahili, utunzi wa mashari, kucheza ngoma za asili na muziki wa dansi, mashindano ya methali, vitendawili na nahau pamoja na malumbano ya hoja motomoto. Matukio mengine yaliyoambatana na hafla hiyo yalikuwa ni pamoja na hotuba mbalimbali; mahojiano maalumu ya Mhe. Balozi Anisa K. Mbega, Balozi wa Tanzania nchini india na Shirika la Utangazaji la India (All India Radio) ambapo mahojiano hayo yalirushwa moja kwa moja wakati wa hafla hiyo kupitia Idhaa ya Kiswahili ya shirika hilo inayojulikana kama Air Word Service -Swahili; maonesho ya bidhaa na vivutio vya utalii wa Tanzania; Filamu ya Tanzania Royal Tour pamoja na vyakula na vinywaji vya Kitanzania vilivyoandaliwa kwa ajili ya kusheherekea siku hiyo. 

Sambamba na matukio hayo, maadhimisho hayo yalitoa fursa ya kubadilishana mawazo baina ya maafisa Ubalozi na diaspora wa India namna bora ya kuitangaza lugha ya Kiswahili nchini India na maeneo mengine ya uwakilishi.

Katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa hafla hiyo, Balozi Anisa  aliwashukuru wageni wote pamoja na wadau kwa kushiriki na kufanikisha maadhimisho hayo ambayo yamefanyika kwa mara ya kwanza tangu ilipotangazwa na UNESCO kuwa tarehe 07 Julai ya kila mwaka ni Siku ya Kiswahili Duniani. Aidha, Balozi Anisa aliwapongeza washiriki kwa kuwasilisha mashairi, methali, vitendawili, nahau pamoja na  mada nzuri katika malumbano ya hoja motomoto kwa kutumia kiswahili fasaha ikiwa ni kielelezo cha mapenzi na hamasa kubwa waliyonayo kwa lugha hiyo na akawaomba kuendeleza utamaduni huo na kuitangaza lugha hiyo pamoja na utamaduni wake.

Aidha, Balozi Anisa alitumia nafasi hiyo kuelezea umuhimu wa siku ya Kiswahili duniani. Pia, akaeleza  historia fupi ya Lugha ya Kiswahili tangu kuanza kutumika kwake kabla na baada ya uhuru na kuenea kwake sehemu mbalimbali hadi kutambuliwa na Umoja wa Mataifa kupitia UNESCO kuwa miongoni mwa lugha 10 yenye wazungumzaji wengi duniani wapatao milioni 200. Aidha, alieleza kuwa kiswahili ni mojawapo ya lugha rasmi nane zinazotambulika na Umoja wa Mataifa kwa kupewa hadhi ya kuwa na Siku yake Maalum ya kuadhimishwa kimataifa na akabainisha kuwa lugha nyingine saba zenye hadhi hiyo ni pamoja na lugha ya Kiingereza (23 Aprili); Kifaransa (20 Machi); Kichina (20 Aprili); Kiarabu (18 Disemba); Kireno (05 Mei); Kirusi (06 Juni) pamoja na lugha ya Kispaniola (23 Aprili).

Katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la India, Balozi Anisa alilishukuru shirika hilo kwa kumkaribisha kuzungumza katika siku hiyo muhimu ya maazimisho ya siku ya Kiswahili duniani ambapo alieleza kuwa siku hiyo ni muhimu sana kwa Tanzania, nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Afrika na dunia kwa ujumla. Pia, alilishukuru shirika hilo kwa kuipa kipaumbele lugha ya kiswahili na kuwa na idhaa mahususi ya lugha ya Kiswahili ambayo utumika kutangaza vipindi mbalilbali nchini India. Aidha, alieleza kuwa, uwepo wa idhaa hiyo ya Kiswahili ni ishara tosha ya uhusiano mkubwa uliojengeka kati India na Tanzania pamoja na nchi za Afrika zinazozungumza kwa lugha ya kiswahili.

Vilevile, alipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada zake za kuiendeleza, kuieneza na kuitangaza lugha ya kiswahili duniani kote na akaeleza kuwa sasa Serikali inaandaa Mpango Mkakati wa Kuibidhaisha Lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania. Akaeleza kuwa ni kwa muktadha huo, ubalozi umejipanga kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kuanzisha vituo vya kufundishia kiswahili katika balozi zake zilizopo nje ya nchi. 

Aidha, Balozi Anisa kwa umuhimu wa kipekee alimuenzi na kumshukuru sana Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuwa Mwasisi wa lugha ya Kiswahili ambayo ilituunganisha na kuwa wamoja na kuishi kwa amani na mshikamano ambazo zimekuwa tunu za kipekee kwa taifa letu la Tanzania.

Balozi Anisa alihitimisha hotuba yake wakati wa hafla hiyo kwa kuwaomba wadau na diaspora walioshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili wakiwemo wanafunzi kuendelea kushirikiana na kufanikisha azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea na jitihada za kuiendeleza, kuieneza na kuitangaza lugha ya kiswahili nchini India na maeneo ya uwakilishi.