Mumbai, Mei 04, 2022 - Ubalozi wa Tanzania nchini India kwa mara ya kwanza umepokea meli ya kwanza iliyobeba Kontena la Parachichi kutoka Tanzania. Kontena hilo liliwasili katika Bandari ya Jawalar Nehru mjini Mumbai tarehe 4 Mei 2022 na kupokelewa na Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa Mbega ambapo mapokezi hayo yalifuatiwa na hafla fupi ya kukata utepe kuashiria mapokezi ya kwanza ya kontena hilo kutoka Tanzania.

Kontena hilo limeingizwa nchini India na Kampuni ya IG Fruits ya India wakishirikiana na Kampuni ya Avoafrica yenye ofisi zake Makambako Iringa.

Akiwa katika hafla ya mapokezi ya kotena hilo, Balozi Anisa alieleza kuwa, kotena hilo lilikuwa lina ukubwa wa futi 40 likiwa limebeba trei 5,700 za parachichi ambapo kila trei ilikuwa na uzito wa kilo 4.

Aidha, Balozi Anisa alieleza kuwa, wafanyabiashara wa India wamehamasika kutokana na juhudi za uhamasishaji zinazofanywa nchini humo na Ubalozi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na sasa wapo tayari kuanza kuingiza matunda aina ya nanasi na embe kutoka Tanzania.

“Huu ni mwendelezo wa juhudi za Ubalozi kwa kushirikiana na Serikali na TAHA wa kuendelea kutafuta masoko ya bidhaa za mazao ya mbogamboga na matunda nchini India. Wafanyabiashara wa India wamehamasika na sasa wanakamilisha taratibu za kuanza kuingiza nanasi na embe za Tanzania nchini India, alieleza Balozi Anisa”.

Vilevile, Balozi Anisa alikishukuru Chama cha Wakulima wa Mbogamboga na Matunda Tanzania (TAHA) kwa ushirikiano wao uliofanikisha shehena hiyo ya Parachichi kuwasili India salama.

Itakumbukwa kuwa, hapo awali Tanzania iliigiza shehena ya kilo 200 za parachichi ya Tanzania nchini India kwa kutumia Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kwa ajili ya kulitambulisha zao hilo nchini India baada ya Serikali ya India kutoa kibali cha kuingizwa kwa zao hilo nchini India mnamo mwezi Novemba 2021.