Tarehe 17 Septemba 2020 Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka H. Luvanda amesaini na kukabidhiwa rasmi hati miliki ya ardhi kutoka Serikali ya India. Ardhi hiyo ni eneo la ukubwa wa mita za mraba 2120.60 (square metres) ndipo lilipo jengo la ofisi ya Ubalozi pamoja na jengo jingine linalotumika kama makazi ya watumishi watatu (3) wa Ubalozi.

Hafla ya uwekaji saini na makabidhiano ya hati hizo imefanyika katika ofisi za Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Miji ya India.

Akipokea hati hizo, Balozi Luvanda ameishukuru Serikali ya India kwa kukabidhi hati hizo, hatua ambayo inathibitisha uhusiano mzuri uliojengeka kati ya nchi hizi mbili.

Kwa upande wake Naibu Afisa Mkuu wa Ardhi wa Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Miji ya india, Bwana Satish Kumar Singh amesifu uhusiano mzuri wa kihistoria uliopo kati ya India na Tanzania na kueleza kuwa, hiyo ndiyo sababu India imeona fahari kubwa kuipa Tanzania eneo la kumiliki katika sehemu mahsusi ya Jumuiya ya Kidiplomasia (Diplomatic Enclave).

Ni sera na mkakati wa Serikali kuhakikisha kuwa balozi zote zilizopo katika maeneo ya kimkakati zinakuwa na majengo na nyumba za watumishi ili kuipunguzia Serikali gharama kubwa za kupanga majengo na nyumba hizo.

Katika hafla hiyo Balozi Luvanda aliambatana na maofisa ubalozi, Bibi Natihaika Msuya na Dkt. Kheri Goloka.

  • Naibu Afisa Mkuu wa Ardhi wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Miji ya India, Bwana Satish Kumar Singh akimkabidhi Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Baraka Luvanda hati miliki ya ardhi ya jengo la Ubalozi, jijini New Delhi tarehe 17 Disemba 2020.
  • Picha ya jengo la Ubalozi wa Tanzania Jijini New Delhi, India.