New Delhi, Juni 16, 2022 - Balozi Caesar C. Waitara, Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amekutana na kufanya kikao cha pili cha mashauriano kwa ngazi ya Wakurugenzi na Balozi Punnet Roy Kundal, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Wizara ya Mambo ya Nje ya India. Mashauriano hayo yalifanyika tarehe 16 Juni 2022 katika Wizara ya Mambo ya Nje ya India mjini New Delhi.

Lengo la kikao hicho pamoja na mambo mengine ilikuwa ni kupitia maeneo ya ushirikiano kati ya Tanzania na India katika sekta mbalimbali zikiwemo Maji, Elimu, Afya, TEHAMA, Utamaduni, Mikopo yenye masharti nafuu, Misaada, Tume ya Pamoja ya Biashara, Tume ya Pamoja ya Kudumu, Mafunzo, kubadilishana uzoefu, Uwekezaji na Biashara, Utalii, Kilimo, Ulinzi na Usalama na mapitio ya Mikataba ambayo haijasainiwa na pande zote mbili. Pia, walijadiliana kuendelea kushirikiana katika masuala mbalimbali ya Kikanda na Kimataifa.

Pande zote mbili zimekubaliana umuhimu wa kuendelea kufanya ziara za viongozi wa juu wa Serikali kwa lengo la kuendeleza na kudumisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili. Kadhalika, ujumbe wa Tanzania uliiomba Serikali ya India kupitia Taasisi ya Mambo ya Nje ya India (Foreign Service Institute) kuandaa kozi maalum kwa ajili ya watumishi wa Wizara kwa upande wa ukalimani (Translation), ujuzi katika majadiliano (negotiation skills), na uandikaji wa hotuba (Speech writting) ambapo ombi hili lilipokelewa na kukubaliwa na Serikali  ya India. 

Aidha, walijadiliana namna ya kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano katika Ujenzi wa reli ya kisasa, uchumi wa buluu, bandari na nishati ya jua. Katika mazungumzo hayo Balozi Waitara aliambatana na Mhe.  Anisa Mbega, Balozi wa Tanzania nchini India, Bi. Natihaika Msuya - Afisa Ubalozi, Dkt. Kheri Goloka – Afisa Ubalozi na Mwambata Afya wa Ubalozi na Bw. Germanus Moris, Afisa Dawati la India. Aidha, kwa upande wa India Balozi Punnet Roy Kundal aliambatana na Dkt. Prakash Shelati.

Vilevile, pande zote mbili zimeridhika na uhusiano mzuri wa muda mrefu wa kidiplomasia uliopo pamoja na mwenendo mzuri wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na India ambapo ujazo wa biashara (Trade volume) umefikia kiasi cha Dola za Marekani 4.5 bilioni na urari wa biashara (Trade balance) ukiwa sawa kwa pande zote.

Katika majadiliano hayo pamoja na mambo mengine, Balozi Waitara aliishukuru Serikali ya India kwa misaada mbalimbali inayotolewa katika sekta ya Afya, Elimu, Ulinzi, fursa za ufadhili wa masomo ya muda mfupi na mrefu na Mikopo yenye masharti nafuu hususan katika miradi ya maji yenye thamani ya kiasi cha zaidi ya shilingi Trilioni 2 iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa katika miji mbalimbali nchini.