Kaimu Balozi wa Tanzania nchini India, Bi. Badriya Kiondo alikuwa na mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya pareto nchini Tanzania [Pyrethrum Company of Tanzania Ltd  - PCTBw. Widmel Mushi ambaye aliutembelea Ubalozi tarehe 23 Julai, 2012.

Baada ya kusalimiana, Bw. Mushi  alimshukuru Kaimu Balozi kwa kukubali kukutana naye mbali na shughuli nyingi za kibalozi alizokuwa nazo.

Alisema, pamoja na kuja kuonana naye, kutembelea Ubalozi na kusalimiana na Maafisa waliopo, jambo kubwa lililomleta  Ubalozini India ni kuja kupata ushauri na maelekezo muafaka ya Ubalozi juu ya namna Kampuni yake PCT itakavyoweza kutumia  Makubaliano rasmi yaliyopo ya kibiashara baina ya Tanzania na India katika kuimarisha soko la pareto pamoja na bidhaa nyingine katika nchi hii.

Aidha, Bw. Mushi ambaye kabla kufika Ubalozini, alifanya ziara katika Miji ya Mumbai [Maharashtra] na Hyderabad [Andhra Pradesh], aliielezea India [Bombay Chemical] kuwa ni mnunuzi mkubwa wa madawa asilia ya kuulia wadudu yanayotengenezwa na Tanzania na kwa mnsaba huo, Kampuni yake imeandaa mkakati wa kuyashawishi  Makampuni makubwa ya Wahindi kwenda  kuwekeza nchini Tanzania katika uzalishaji/ukamuaji wa zao la pareto.  

Alisema Mkakati huo ukifanikiwa si kama tu utainua sekta ya uwekezaji nchini  bali vile vile utasaidia kupanua zaidi soko la Tanzania nchini India, [ina mahitaji makubwa ya madawa asilia ya kuulia wadudu yanayotokana na pareto] na hivyo kupunguza “trade imbalance” iliyopo kati ya Tanzania na India.

Mkurugenzi huyo wa PCT alisema kwamba tayari ameshafanya mazungumzo ya msingi na baadhi ya Makampuni ya India  katika Miji aliyotembelea na kwamba ana matumaini makubwa ya kufanikiwa kwa juhudi hizo. Bw. Mushi ameahidi kuuarifu Ubalozi kwa kila hatua itakayochukuliwa na Kampuni yake kuendeleza juhudi hizo na nyenginezo zitakazofuatia.

Akitoa muhtasari wa utendaji na mafanikio ya PCT, Bw. Mushi alisema Kampuni yake  ambayo  mwaka 2006 iliingia ubia na Kampuni McLaughlin Gormley King Company [MGK]   inaendesha shughuli za ukamuaji wa madawa [asilia] ya kuulia wadudu kutokana na zao la pareto.

Alisema MGK inaendesha mradi muda mrefu [long term project]  wa kuimarisha kilimo cha pareto pamoja na kuinua kiwango cha ubora wa dawa za kuulia wadudu zinazotokana na zao hilo nchini Tanzania. Katika kuendeleza mradi huo, PCT ina mashamba  makubwa ya pareto Arusha pamoja na kiwanda cha kukamulia pareto huko Mafinga, Iringa,  vile vile inaendesha kampeni za  kuwahamasisha wakulima wadogo wadogo kulima zaidi zao hilo pamoja na  kununua mazao [pareto] kutoka kwa wakulima hao.

Madawa hayo ya kuuliwa wadudu yanayotengezwa na PCT ambayo hayana athari kwa mazingira, mazao wala mtumiaji na yenye ubora wa hali ya juu  huuzwa zaidi Marekani chini ya udhamini wa MGK na kwamba mwaka 2011 Tanzania [TCP] imeuza nchini Marekani Madawa hayo yenye thamani ya zaidi ya Dola la Kimarekani milioni 60.  na vile vile madawa hayo yana soko kubwa katika nchi mbali mbali za Ulaya na Asia hasa   India.

Naye Kaimu Balozi Bi. Badriya Kiondo,alimshukuru na kumpongeza sana Bw. Mushi kwa moyo wake wa kizalendo pamoja na  juhudi zake zenye lengo la kuiletea maendeleo Tanzania.

Alisema amefarajika sana kukutana na kubadilishana mawazo na yeye Mtanzania wenye mawazo/mipango mizuri na nia njema ya kuiendeleza nchi yetu na kwamba Ubalozi utakuwa tayari kutoa msaada unaostahiki kwa mujibu wa sheria na taratibu husika ili kuhakikisha kwamba  juhudi hizo zinazaa matunda kwa manufaa ya taifa letu.

Kaimu Balozi alimueleza Bw. Mushi kwamba Tanzania na India zimetiliana saini Mikataba/ makubaliano kadha yenye lengo la kuendeleza ushirikiano mwema uliopo baina ya nchi hizi katika nyanja mbali mbali.

Bi Kiondo alitaja baadhi ya Makubaliano ya kibiashara  kuwa ni Mkataba  wa kuepuka utozwaji wa kodi mara mbili [Double Taxation Avoidance Agreement DTAA] ambao kwa mara ya kwanza ulitiwa saini mwaka 1979 na kuboreshwa mwaka  2011. Aidha, alisema  tangu mwaka  2009 Tanzania inafaidika na  Mpango wa  mshamaha/unafuu wa kutozwa  ushuru wa bidhaa  [Duty Free and Tariff Preference - DFTP]  uliotolewa na Serikali ya India kwa nchi zinazoendelea kwa bidhaa zinazouza nchini humu.

Kaimu Balozi alimwambia Mkurugenzi huyo wa PCT kwamba Tanzania imeruhusiwa kuuza India zaidi ya bidhaa 90 chini  mpango huo na kwamba PCT pia kama Kampuni ya Tanzania inaweza kunufaika na Makubaliano hayo. Bw. Mushi ambaye alipatiwa nakala ya orodha ya mazao hayo, ameahidi kuutafakari ili kuona namna Kampuni yake itakavyoweza kufadika nao kwa mujibu wa sheria na kanuni husika.

Wakizungumzia suala  la kuwepo kwa soko kubwa la India [watu Bilioni 1.2] kwa mazao na bidhaa mbali mbali za Tanzania, Kaimu Balozi na Mkurugenzi wa PCT wamebaini kwamba Watanzania hawana budi kubabdilisha mtazamo [mindset] zao juu ya India kwa kuchukua hatua za makusudi za kushiriki kikamilifu katika mikutano, makongamano, maonyesho nk. yanayofanyika India ili kupata wawekezaji, washirika wa kibishara, kuanzisha na kupanua masoko ya bidhaa zao hususan mazao ya kilimo.

Bw. Mushi ameahidi kusaidia juhudi za Ubalozi kuwaelimisha Watanzania, hasa Sekta binafsi kuhusu umuhimu wa India kwa uchumi wa Tanzania  vile vile ataendelea kuushirikiana na Ubalozi katika kusukuma mbele maendeleo ya Tanzania.

Bw. Mushi, vile vile ni Mkurugenzi Mshauri wa  Kampuni zinazohusiana na mazao ya kilimo za Agri Solution Africa Ltd. [AXSOL]; Sunflower Development Company [SDC]  na Longbridge Edible Oil Company [T] Ltd [LEO]

Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Afisa wa Ubalozi anayeshughulika na masuala ya uchumi na biashara Bi. Leluu Abdallah.