Singapore, Novemba 18, 2021- Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango tarehe 18 Novemba 2021 alitembelea Bandari ya nchi ya Singapore na kujionea jinsi bandari hiyo inavyofanya kazi.

Katika ziara hiyo Makamu wa Rais alishuhudia teknolojia mbalimbali zinazotumika katika kufanya kazi katika bandari hiyo ikiwemo upakuaji na upakiaji makasha na mizigo, ukaguzi wa mizigo pamoja na ufuatiliaji makasha wakati wote yanapokuwa safarini.

Akitoa maelezo namna bandari hiyo ilivyopiga hatua kubwa katika kipindi cha muda mfupi makamu wa Rais wa Mamlaka ya Bandari ya Singapore anayeshugulikia masuala ya biashara Bwana Ong Seow Leong alieleza kuwa bandari hiyo imewekeza katika mafunzo pamoja na ubunifu uliopelekea kuongezeka kwa teknolojia inayotumika hivi sasa katika kutoa huduma ikiwemo kuweza kufanikiwa kushusha na kupakia makasha laki moja ndani ya siku moja.

Aidha, alieleza kuwa Bandari ya Singapore imekua na mtandao na bandari zingine duniani hivyo kuongeza ufanisi wa ufanyaji kazi wa bandari hiyo. Vilevile, akaeleza kuwa Bandari ya Singapore imekuwa ikiweka mkazo katika kutafuta masoko pamoja na kufanya tafiti zinazoweza kuongeza watumiaji wa bandari hiyo.

Katika hatua nyingine Bwana Leong alieleza kuwa ni lazima kuwepo na mipango ya muda mrefu katika uendeshaji wa bandari na tayari nchi ya Singapore inaendelea na ujenzi wa bandari mpya na ya kisasa ambayo kwa miaka ijayo itaweza kutoa huduma kwa ufanisi zaidi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango alieleza kuwa Tanzania itashirikiana na Uongozi wa Bandari ya Singapore katika kutoa mafunzo kwa watumishi wa bandari za Tanzania pamoja na kupeleka watalaamu wa bandari kutoka Singapore kwenda Tanzania ili kushirikiana katika kufanya maboresho ya haraka hasa bandari ya Dar es salaam.