Hotuba Ya Balozi Baraka H. Luvanda Wakati Wa Mahafali Ya Wanafunzi Na Wanachama Wa Umoja Wa Wanafunzi Wa Mysore (TASAM),17 Machi,2018.

Ndugu Rais wa TASAM na Mwenyeji wetu,

Ndugu Viongozi katika Meza Kuu,

Ndugu Wageni Waalikwa,

Ndugu Wahitimu,

Marafiki wa TASAM,

Mabibi na Mabwana,

Asalaam Aleykum,
Namaskar,
Bwana Asifiwe,
Tumsifu Yesu Kristo.

 

Ndugu Rais,

Kama ulivyokwisha kudokeza katika hotuba yako, leo sio siku ya kupoteza muda kwa kusikiliza hotuba ndefu. Nami ninaitikia mwongozo wako kwa kuongea kwa ufupi.

Kwanza kabisa ni shukrani. Ninawashukuru sana kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika kufurahia wenzetu kuweza kutimiza lengo na dhumuni lililokuwa limewaleta India. Hongereni sana wahitimu wote.

Aidha, nawapongeza na kuwashukuru wakufunzi wenu waliowapatia elimu, ujuzi na maarifa na kuwawekeni katika hali ya utayari kwenda kukabiliana na changamoto za maisha yanayoanza leo.

Ndugu Rais,
Wageni Waalikwa,
Ndugu Wahitimu,

Mahafali ni tukio laa kipekee sana popote pale. Kwa wahitimu, tukio ni muda mahsusi wa kusherehekea, ni muda pekee wa kutathimini mafanikio ya masaa mengi waliyotumia katika kuhakikisha wanafikia malengo yao. Lakini pia siku kama ya leo mara sherehe hizi zinapohitimishwa ni muda kwa wahitimu kutafakari ukurasa mpya wa maisha. Mlango wa dunia unafunguka na furaha, maumivu na wajibu mpya. Nayasema haya si kwa kuwaogopesha, bali hiyo ndiyo hali halisi inayowakabili.

Ndugu Rais,
Ndugu Wahitimu,
Mabibi na Mabwana,

Wahitimu wetu hawa wamefanya jitihada kubwa hadi kufikia siku ya leo. Lakini pia ni ukweli kuwa wazazi wao wametekeleza wajibu wao vizuri wa kuhakikisha mazingira rafiki yamekuwepo wakati wote wa safari yao ya masomo. Wakufunzi halikadhalika wamekuwa sehemu ya mafanikio haya. Kwa ajili ya kuwapongeza wote niliowataja, naomba tupige makofi mengi.

Ndugu Rais,
Wageni Waalikwa,

Takwimu zilizopo zinaonesha kuwa kila mwaka Tanzania inazalisha wahitimu wapatao laki nane na wote hao wanaingia katika soko la ajira. Changamoto kubwa imekuwa ni ufinyu wa ajira zenyewe iwe kwa sekta ya umma au kwa sekta binafsi. Na mbaya zaidi kwa upande wa sekta binafsi ni kuwa na ajira zisizodumu. Ninalitaja jambo hili kwenu ili kuwaandaa kisaikolojia

Baadhi yenu watakuwa na matarajio ya kuajiriwa. Hakuna shaka kuwa watapata ajira baada ya kuhangaika sana. Lakini sina uhakika kama mmeshakutana na neon "Ujasiriamali."Na kama linafahamika miongoni mwenu basi naamini mtakuwa mmejiweka vizuri kukabiliana na changamoto za kimaisha zinazoanza leo. Kwa wale ambao kwa bahati mbaya hawakuwahi kukutana na neno hili nawasihi watumie simu zao kubofya na kupata maana yake watanufaika sana na maelezo na mifano inayotolewa.

Ndugu Rais,
Wageni Waalikwa,
Ndugu Wahitimu,

Kwa kuwa niliahidi kuitikia rai ya kutumia muda mfupi, naomba nimalizie nasaha zangu kwa kuongezea yafuatayo:

Matarajio ya wazazi wenu ni makubwa, matarajio ya wadogo zenu ni makubwa, matarajio ya nchi ni makubwa na hata matarajio ya familia zenu pia ni makubwa. Na kama ilivyokwishakusemwa,ninanukuu: "Our prime purpose in life is to help others. And if you can’t help them, at least don’t hurt them." Nikiwaangalia nyuso zenu sioni hata mmoja wa kumuumiza mtu aliyechangia kumfikisha hapa siku ya leo.

Na kwa kuhitimisha, naomba nitoe rai hii. Mmehitimu ngazi hii ya elimu na katika fani mbali mbali hii. Sote tunajumuika kukupongezeni sana. Lakini ninashawishika kuamini kuwa wengi wenu bado mna hamu na uwezo kujiendeleza zaidi ya hapo.

Nawasihi fursa ya kujiendeleza zaidi ikijitokeza ichangamkieni bila kusita. Kwani ni ukweli usiofichika kuwa when you buy a car or a piece of equipment it comes with a user’s manual with maintenance instructions. You have to service it regularly to ensure it continues to serve you well. How much more important is it to regularly service your brain after graduation? I know there are graduates who find no time to read a book again after graduation Don’t be like that. For, a mind is like a garden. If it is not watered, and cultivated, weeds will take over.

Kwa mara nyingine, nawashukuruni sana kwa kunialika katika furaha hii na ninaamini kuwa huu ni mwanzo tu.

Asanteni sana kwa kunisikiliza.