New Delhi, Machi 28, 2022- Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Balozi Anisa Mbega ameupokea Ubalozini Ujumbe wa kikundi cha ngoma za asili cha Nyati Mchoya kutoka katika Kijiji cha Nzali, Chamwino, jijini Dodoma, ambao wamekuja nchini India kushiriki Tamasha Maarufu la Kimataifa la Utamaduni na Sanaa la Surajkund Internation Crafts Mela 2022 Katika mji wa Faridabad katika Jimbo la Haryana tangu tarehe 18 Machi 2022. Mhe. Balozi Anisa amekipongeza na kukishukuru Kikundi hicho kwa kuiwakilisha vyema nchi yetu kwenye Tamasha hilo katika fani ya ngoma na kuwahamasisha waongeze bidii zaidi katika kutangaza utamaduni wa Tanzania pamoja na bidhaa zake katika matamasha mengine kama hayo. Ikiwa ni mojawapo ya harakati za kutangaza vivutio vya utalii wa Tanzania.

Aidha, Mhe. Balozi Anisa aliwakaribisha Ubalozini na kujumuika nao kwa chakula cha mchana ambapo alitumia fursa hiyo kubadirishana machache juu ya namna ya kuimarisha na kuendeleza ushirikiano katika kuutangaza utamaduni wa Tanzania na vivutio vyake.

Vilevile, baada ya hafla ya chakula cha pamoja, kikundi hicho kilitumbuiza mbele ya Mhe. Balozi na Maafisa Ubalozi wakiwa na familia zao ambapo walijumuika kwa pamoja kucheza na kuimba ngoma za asili za Tanzania.

Mwisho, Mhe. Balozi Anisa alikishukuru kikundi hicho na kukiomba kuendelea kushirikiana na Ubalozi katika kuitangaza vyema Tanzania katika matamasha kama haya na mengine yatakayojitokeza.