Rajkot, Machi 20, 2022-Balozi wa Tanzania nchini India, Mhe. Anisa K. Mbega amemtembelea na kumjulia hali mwanafuzi, Bi. Janeth Sitta Tungu aliyelazwa katika hospitali ya Gokul iliyoko mjini Rajkot katika Jimbo la Gujarat. Bi. Janeth ni mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya kwanza (B.Sc. Pharmacy) anayesoma katika Chuo Kikuu cha RK kilichopo Rajkot ambapo tarehe 16 Februari 2022 aligongwa na gari wakati akivuka barabara na kujeruiwa vibaya katika sehemu mbalimbali mwilini. Baada ya ajali hiyo Bi. Janeth alikimbizwa hospitalini hapo kwa msaada wa wanafunzi wenzake wa kitanzania akiwa na hali mbaya ambapo madaktari wa hospitali hiyo waliweza kuokoa maisha yake kwa kumpatia tiba stahiki.

Pamoja na kumpa mkono wa pole, Balozi Anisa amemuombea Bi. Janeth kupona haraka ili aweze kuendelea na masomo yake.

"Nilishtushwa sana na taarifa za ajali hile mbaya, lakini sasa nafurahi kukuona ukiwa mwenye afya nzuri ikilinganishwa na taarifa nilizozipata hapo awali, nakupa pole sana na nikuhakikishie Serikali kupitia Ubalozi itasimamia na kugharamia matibabu yako" alisema Balozi Anisa wakati akimjulia hali hospitalini hapo. Aidha, Mhe. Balozi Anisa aliwashukuru wanafunzi wa kitanzania wanaosoma katika vyuo vilivyopo Rajkot kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha katika kumsaidia na kumuuguza mwenzao na kuwataka waendelee na moyo huo huo wa upendo wa kusaidiana katika shida na raha. Vilevile, aliwashukuru madaktari pamoja na uongozi wa hospitali ya Gokul kwa kuokoa maisha ya mwanafunzi huyo kwa kumpatia tiba bora.

Kwa upande wake Bi. Janeth na mama yake ambaye aliwasili India hivi karibuni kuja kumuuguza mtoto wake kwa pamoja walimshukuru Balozi Anisa kwa ukarimu na upendo aliouonesha kwa kuwatembelea hospitalini hapo, na wakaishukuru sana Serikali kwa kuwajali pamoja na kugharamia matibabu ya mtoto wake. “Kwa kweli naishukuru sana Serikali kwa kutupa msaada huu mkubwa wa kugharamia matibabu ya mtoto wetu, mimi ni mkulima na baba yake ni mstaafu, kwa kweli bila ya serikali yetu tukufu kutusaidia tusingeweza kugharamia matibabu ya mtoto wetu”, aliongeza Bibi Tungu.

Balozi Anisa aliambatana katika ziara hiyo na Mwambata wa Afya wa Ubalozi, Dkt. Kheri Goloka ambaye amekuwa akifuatilia kwa ukaribu pamoja na kuratibu matibabu ya mwanafunzi huyo.

Akiwa mjini Rajkoti, Balozi Anisa Mbega alikutana na wawakilishi wa wanafunzi wa kitanzania na kufanya nao mazungumzo ambapo aliwapongeza sana  kwa jinsi wanavyoshirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabiri hususan, katika tukio hili la ajali mbaya aliyoipata mwanafunzi mwenzao na kuwaomba waendelee na moyo huo pamoja na kuongeza juhudi kwenye masomo yao.

Aidha, tarehe 21 Machi 2021, Balozi Anisa alikutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Chuo Kikuu cha Marwadi cha mjini Rajkot ambacho kina wanafunzi wa kitanzania takribani 175 ambapo, pamoja na mambo mengine, aliushukuru uongozi wa Chuo hicho kwa kuwapokea wanafunzi 45 wa kitanzania wanaosoma chuoni hapo kwa ufadhili wa Serikali ya India.